IDADI YA WAKAZI
Sehemu kubwa ya wakazi wa Tanzania ni Waafrika, 95% ikijumuisha makundi 8 ya kiasili, yakiwa na vikundi vidogo vidogo zaidi ya 130. Lugha 120 zenye kujitegemea zinadhihirisha tofauti za kitamaduni ndani ya nchi. Lugha rasmi za kitaifa ni Kiswahili na Kiingereza. Idadi ya wakazi ni milioni 36, kati yao 40% wako chini ya miaka 14. Wastani wa makadirio ya matarajio ya miaka ya kuishi ni 45.
Idadi ya wakazi wa maeneo yanayoizunguka Ifakara hujumuisha zaidi makabila 3; Wapogoro, Wandamba na Wambunga, wakitegemea kwa namna ya pekee zaidi kilimo na uvuvi. Kilimo cha mpunga, mahindi, miwa, ngano na pamba yenye kiwango cha juu cha ubora, kwa sehemu kubwa ina msingi wake katika mfumo wa uchumi toshelezi. Hii ni nafasi ya pekee ambapo wakazi wa vijijini huweza kujikimu, kwani gharama za chakula humeza karibu 70% ya wastani wa pato la familia. Mbogamboga hasa maharage, mihogo, viazi na mchicha, na matunda kama ndizi na maembe hustawishwa zaidi. Mazao huoanishwa na njia za asili za kilimo zinazoshamiri, njia za kilimo za kipindi kabla ya ujio wa viwanda, na hutegemea kwa kiasi kikubwa mvua za masika. Ingawa eneo lina rutuba ya kutosha, serikali na mashirika ya misaada hulazimika kuchangia utoaji wa chakula katika miaka yenye uhaba wa mvua. Kinyume chake kinaweza pia kutokea. Mara kwa mara mafuriko yatokanayo na mito Kilombero na Lumemo huharibu mazao, barabara na madaraja.
Katika miaka iliyopita, makabila yenye asili ya ufugaji wa kuhamahama kama Wamasai, Wasukuma na Wamang’ati wamehama kwa ongezeko kubwa kutoka kaskazini mwa Tanzania. Makabila haya hutegemea sana ufugaji na hivyo humiliki kiasi kikubwa cha mifugo. Migogoro na wakazi wa maeneo haya haiwezi kuepukwa, kwani wanyama huharibu mazao na kingo za mto Kilombero.


